Imeandikwa na Ahmed Karama
Mji wa Amu, eneo lenye historia tajiri, utalii na urithi wa kipekee wa waswahili unakumbwa na changamoto ya upatikanaji wa maji Safi na salama. Kwa miaka mingi, shida ya maji imeendelea kuwa kero sugu kwa wakaazi wa mji wa Amu haswaa wale wanaoishi mtaa wa Mililani.
Inasikitisha sana kuona Kuna baadhi ya watu wanalalamikia uhaba wa maji katika taifa huru kama Kenya. Tunasema maji ni uhai, Sasa inakuaje baadhi ya watu wakose haki hii ya uhai unaopatikana kutoka kwa maji?
Suala la uhaba wa maji si jambo geni kwa wakaazi wa mji wa Amu lakini kwa wale wanaoishi eneo la milimani neno maji ni kama limeingia kimakosa katika kamusi ya kiswahili.
Baadhi ya maeneo wakilalamikia uhaba wa maji, wakaazi wa milimani hawapati maji kabisaa, yaani mita za maji zimekaa kama mapambo katika majumba yao. Kwa kweli wakaazi hawa wanawaonea wivu watu wa mitaa mingine ya mji wa Amu ambao wanapata maji japo Mara moja ama mbili kwa wiki. Kuongeza chumvi kwa kidonda, watu hawa hawapati maji ambayo ni haki yao ya kimsingi lakini kila mwezi wanaletewa bili ya maji ya takriban shilingi Mia tatu na hamsini.
Kampuni ya usambazaji maji lamu (LAWASCO) wameyathibitisha madai haya na kujitetea kuwa eleo la milimani halipati maji kwa sababu ni eneo ambalo liko juu hivyo basi maji hayapandi. Hata hivyo mkurugenzi mkuu wa LAWASCO ameelezea changamoto chungu nzima zinazowakumba ambazo zinawarudisha nyuma katika kutoa huduma bora za maji kwa watu wa kaunti ya lamu. Kampuni hiyo kupitia kwa mkurugenzi mkuu waliahidi kulishughulikia tatizo hilo na wanasubiri ufadhili kutoka kwa kaunti ya lamu ili waweze kulitatua tatizo hilo jambo ambalo halijafanyika takriban mwaka mzima sasa.
Shida ya maji lamu si jambo jipya, bali ni tatizo linalohitaji hatua za haraka na za pamoja. Bila upatikanaji wa maji Safi, maendeleo ya kijamii na kiuchumi hayatapatikana. Serikali kuu, serikali ya kaunti, mashirika ya kibinafsi na wananchi kwa jumla Wana jukumu la kuhakikisha kuwa maji Safi ambayo ni haki ya msingi ya binadamu yanapatikana kwa kila mmoja na kila wakati.
Tusisahau maji ni uhai.