WritAfrica

Imeandikwa na Ahmed Karama

Kwa muda mrefu wanasiasa nchini Kenya wamekuwa wakiwatukana wakenya. Wakenya ambao ndio walipa ushuru na ambao ndio wapiga kura wanaowaajiri wanasiasa hawa katika nyadhifa tofauti tofauti.  Inakuaje muajiriwa kumtukana muajiri? Swali langu lisikushangaze sana kwani ndio hali halisi iliyopo katika taifa la Kenya. 

Labda unajiuliza Kwani wanasiasa wanawatukana vipi walipa ushuru wa Kenya? Naam nitalijibu swali hili kwa ufupi na ufasaha . Wakenya ndio walipa ushuru ambao unatumika kuwalipa wanasiasa walioshikilia nyadhifa mbalimbali kuanzia rais mpaka mwakikishi wadi. Wakenya hawahawa pia ndio wapiga kura ambao hurauka asubuhi na mapema kabla jogoo hajawika kupiga foleni katika vituo vya kupiga kura ili kuwachagua wawakilishi ambao wanawapa kandarasi ya miaka mitano wakiwa na matumaini ya kusaidiwa kubadilisha hali zao za maisha. Sasa nikisema wakenya ndio waajiri na “viongozi”, ambao baadae hubadilika kuwa wanasiasa, ndio waajiriwa nitakuwa nimekosea?

Naomba tusaidiane kuitafakari hii hali, inawezekanaje muajiri kutoka kwake asubuhi na mapema, labda hata bila ya kifungua kinywa na wakati mwengine bila hata viatu, kuenda kupiga foleni na kumpa ajira mtu ambae wakati huo yupo kitandani anang’orota na atakapoamka anywe chai yake nzito alafu baadae aende katika kituo cha kupiga kura na gari ilhali waliorauka kumpa  kazi wametembea kwa miguu. Je haya kama si matusi ni nini?

Taswira kama hiyo niliyotoka kuielezea imejitokeza tena juzi, tarehe saba, mwezi wa saba, mwaka elfu mbili ishirini na tano katika kisiwa cha pate na amu kaunti ya Lamu. Siku hiyo ya sabasaba kulifanyika mikutano mikubwa katika kaunti ya lamu, mikutano iliyoongozwa nae naibu Rais wa taifa la Kenya Profesa Kithure Kindiki.

Katika kisiwa cha pate, lamu mashariki wakaazi kutoka maeneo mbalimbali walikusanyika katika mji wa Faza asubuhi na mapema ili kumlaki naibu rais na wanasiasa wengine.  Kama kawaida muajiri alirauka na kutembea kwa miguu ili kuja kumlaki muajiriwa ambaye aliwasili katika mkutano na ndege tena akiwa amechelewa. Je haya si matusi?

Katika mkutano huo wanasiasa mbalimbali walijitapa na kujipiga kifua kwa kuonyesha ubabe wao na uwezo wao wa kifedha kwa kutoa michango hadharani eti wanasaidia kuwainua kina mama kiuchumi(women empowerment) pesa ambazo zimetoka kwa wapiga kura ambao ndio hawa kina mama na Vijaya waliorauka tangu alafajiri ya mungu kuwasubiria ‘waheshimiwa’. Inakuaje ‘bosi’ anachangiwa na wafanyikazi wake ili aweze kuinuka kiuchumi?

Tusi kubwa zaidi Kati ya yote liko hapa, baada ya michango hiyo yote kila kikundi kilikabidhiwa shilingi elfu ishirini na nne na kulingana na sheria kikundi hakitakiwi kuwa na wanachama wanaopungua kumi na watano,  hivyo basi kwa  hesabu ya haraka haraka ni kuwa kila mwanakikundi atapata shilingi elfu moja na Mia Sita za kumwezesha kujiboresha kiuchumi. Hili ni tusi si tusi?

Cha kushangaza zaidi ni kuwa wanasiasa hawa wanapojikusanya na kuwachangia kina mama na Vijana, yupo ‘kiongozi’ aliyechaguliwa anayeitwa mbunge ambae ana pesa za mfuko wa ‘NG-CDF’ na yupo mwengine anayeitwa mwakilishi wa wanawake ambae anasimamia pesa za ‘NGAAF’ ( National Government Affirmative Action Fund), pesa ambazo moja ya majukumu yake ni kuwasaidia kina mama na vijana kuinuka kiuchumi. Kwani hizi pesa zinatumika kufanya nini mpaka wanasiasa wajikusanye kuwachangia wakenya? Kwa nini kusiundwe mbinu na mifumo thabiti ya kuwasaidia waajiri kuinuka kiuchumi bila kuwategemea waajiriwa kuwachangia?

Tags:

No tags assigned to this post.

Related Posts

Top Categories

Trending News

Frozen Future
Kovu cha Kifo
Survival
Death Note
United or Justice
Kiongozi Dhalimu

Subscribe to Our Newsletter

Join our vibrant community of young poets, writers, and illustrators.