Imeandikwa na Ahmed Karama
Suala la udhalimu wa ardhi limekuwa donda sugu katika taifa la Kenya, haswaa mkoa wa pwani. Si Mombasa, si Lamu, si Tanariver, si Kilifi, si Kwale. Licha ya wapwani Kulalamikia suala hili kwa muda mrefu, Vilio vyao vimekuwa kama kumuimbia kiziwi taarabu yaani Serikali ya Kenya wamekuwa hawasikii wala hawaoni, ni sikio la kufa ambalo halisikii dawa.
Katika enzi hizi za maendeleo ya miradi mbalimbali, jamii ya watu wa Lamu na wao hawajaachwa nyuma, wamekumbukwa si haba. Wakaazi wa Lamu walifarijika na kujihisi kama wakenya wengine walipotajiwa kuletewa mradi wa LAPSSET (Lamu Port-South Sudan-Ethiopia-Transport Corridor project) na ujenzi wa bandari ambayo ingekuwa mwanzo wa maendeleo ya kaunti ya lamu na kutatua tatizo la uhaba wa kazi.
Ni takriban miaka kumi tangu kuanzishwa kwa mradi wa LAPSSET na ujenzi wa bandari ya lamu ila nyuso za watu wa lamu haswaa wale wa kililana zinalia badala ya kucheka. Mradi wa LAPSSET ambao ulikuwa wa matumaini kwa wengi sasa umegeuka kuwa jinamizi na jini la kutisha.
Kililana ni eneo ambalo liko lamu magharibi na limekuwa nyumbani kwa jamii ya wakulima, wavuvi na wafugaji kwa miongo mingi. Ni ardhi yenye rutuba na thamani kubwa ila sasa juhudi na ndoto za wakaazi wa eneo hilo zimezimwa ghafla na ujio wa mradi wa ujenzi wa bandari.
Wakaazi wa Kililana wamepoteza ardhi zao kwa kufurushwa katika mashamba yao. Katika mradi wa LAPSSET, jamii ya Kililana haikuhusishwa kikamilifu jambo ambalo ni kinyume na sheria ya ardhi na katiba ya Kenya ambayo inasisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya ardhi yao.
Cha kusikitisha zaidi ni kuwa watu hawa wanafurushwa katika ardhi zao bila fidia na kumekuwa na ripoti za wananchi kutishiwa, kukamatwa kiholela na hata kushambuliwa kwa ajili ya kujaribu kudai haki zao za ardhi.
Jamii hizi zinakodolea macho kupotea kwa utambulisho, mila, desturi na juhudi zao za tangu jadi na kukithiri kwa umaskini kwani ardhi hii ndio chanzo kikuu cha kipato chao.
Dhuluma za ardhi kililana ni kiini cha mateso ya kimya kwa jamii zisizokuwa na sauti. Hili ni suala la haki za binadamu, uhuru wa kikatiba na ustawi wa wananchi. Iwapo taifa linataka kufanikisha maendeleo ya kweli basi lazima litangulize haki, usawa na heshima kwa ardhi ya wananchi.